2/20/2005

POROJO ZA KIJIWENI

Nakumbuka ile siku nilipofika Chicago kwa mara ya kwanza. Miaka miwili iliyopita. Sikupapenda hata kidogo. Mbio sana. Shimeshime. Utu hakuna. Hakuna wa kumsimamisha kumuuliza saa.
Chicago kuna kila kitu. Kuna utajiri uliokithiri na kuna ufukara unaokutoa machozi. Kuna baadhi ya mitaa ukifika unajiona kama uko sokoni Kariakoo. Tena kule shimoni. Na mingine ukienda lazima uwe na roho ya paka. Silaha nje nje. Vibaka kama utitiri. Michoro ya majina na alama za magenge kila ukuta. Milio ya ving'ora vya polisi na risasi kila saa.
Ninapokuwa katika mitaa kama hii huwa najiuliza, "Anayeita Marekani ni ulimwengu wa kwanza anamaanisha kuwa mitaa hii nayo ni ulimwengu huo wa kwanza?" Unajua kuna Marekani nyingi sana. Mapicha ya kwenye magazeti kama Ebony, sinema, filamu za muziki, n.k hupotosha sana kwa kutufanya tuamini kuwa Marekani yote inang'ara. We! Tembea uone.

Naanza kuhisi kuzeeka maana nimeanza kuchukia sana miji mikubwa, majengo makubwa ya orofa, magari yanayokwenda kwa kasi, n.k. Napenda miji midogo yenye mandhari mchanganyiko wa mji na kijiji. Napenda miji-vijiji. Nadhani kwakuwa nimezaliwa kijijini na kwenda shule mjini. Napenda miji yenye miti, mito, nyumba za ukubwa wa wastani, mashamba, milima, bustani, wakulima, ng'ombe, kuku, mbuzi, bata, masoko yenye mazao ya wakulima wadogowadogo, n.k.

Bado niko Chicago. Basi, si unajua wale vijana wanaouzia abiria kwenye mabasi maji, mikate, magazeti, na bidha nyingine pale Bongo? Kuna sehemu kule Chicago namna hiyo. Ninapita hivi mara moyo ukanidunda du! Nikashtuka, ala! Machinga mpaka huku? Jamaa walikuwa wanauzia abiria na watu wengine maji baridi. Nikawasemesha kiswahili maana nilidhani huenda wametoka Bongo. Wakanikodolea macho. Sasa sijui walijikausha au labda ni machinga wa hapa!
Ngoja nibadili usemi. Nilisema sipendi miji mikubwa. Nadhani mji wa Seattle nitautoa katika kauli hiyo. Mji poa mno mno. Seattle. Seattle. Mji maridai. Watu wastaarabu. Ajabu sana ukisikia honi za magari. Karibu kila mtu anatembea barabarani akinywa kahawa. Huu ni mji ambao kila dakika unaweza ukafirikia kuna tukio la kufurahisha linatokea au kuna sherehe fulani. Nikifika pale huwa napoteza muda kwenye maduka ya vitabu, hasa duka la Left Bank Books na pia lazima nitembelea soko la "kariakoo" la Seattle la Pike Place Market ambapo zaidi ya kutazama wauza samaki ambao huwa ni kiburudisho kwa watu wengi kwa jinsi wanavyokata kwa haraka na kurushiana minofu ya samaki wakubwa kama gari aina ya Anglia (sijui kama mnafahamu gari hili la zamani sana!) kwa staili ya pekee, huwa napenda sana kutazama watumbuizaji kadhaa ambao wametapakaa sokoni hapo. Zaidi napenda kumuona msanii huyu hapa aitwaye Artis au Spoonman, ambaye alinipa CD yake mwaka jana baada ya kukaa siku nzima nikimsikiliza! Artis ni mwanamuziki anayepiga muziki kwa kugonganisha vijiko! Muziki anaoutengeneza ukiusikia huwezi amini masikio yako. Ukifika Seattle lazima umtafute Spoonman. Mwingine ambaye huwa lazima nimtafute kila nikienda sokono hapo ni mwanaharakati, mpiga gitaa, na muimbaji Jim Page. Huyu bwana kwangu mimi sio mwimbaji kama watu wanavyomwita bali ni msimulizi wa hadithi. Nyimbo zake ukisikiliza anaongea nawe kama anakusimilia kisa fulani. Na anaandika mashairi acha mchezo. Mtazame hapa.
Nikukumbushe kuwa mji wa Seattle unakumbukwa kutokana na watu waliozaliwa, kuishi, au kufia hapo kama vile Jimmi Hendrix (mlami mweusi aliyemaliza kabisa kupiga gitaa...hakuna kitu kipya cha kupiga tena kwenye gitaa baada ya mlami huyu!), Bruce Lee, Kurt Cobain wa kundi la Nirvana.
New York... kule ndio hata nikiambiwa nikaishi bure siendi. Kutembelea sawa. Sio kukaa.
Kila mtu yuko nyuma dakika tano, kwahiyo kila mmoja ana haraka ya kuwahi mahali. Amechelewa, hivyo mpishe haraka apite.
Kila mtu anataka kukuuzia kitu.
Kila mtu anataka kukuomba senti za sigara.
Kila mtu anataka uingize mkono mfukono. Anataka kukutoa kitu kidogo. Ukikuta mwanamuziki au mchekeshaji anatumbuiza usisimame na kutazama kama huna hela ya kumpa. Hakuna onyesho la bure ndugu yangu. Unataka akale polisi?

Ukitembelea Harlem, kuna mitaa fulani pale unaweza kudhani kuwa uko Dakar, Senegal kwa jinsi walivyojazana Wasenegali. Hii ndio ile mitaa ambayo kabla mwanamuziki hajatoa albamu yake rasmi, jamaa wanakuwa wameshaanza kuiuza! Wanatoa wapi? Usiniulize.
Nikienda New York, kijiwe changu huwa ni Nuyorican Poets Cafe. Kongoli hapa. Au unaweza kunikuta katika duka hili liitwalo Hue-Man Bookstore and Cafe. Unajua kama unanitafuta popote pale nilipo dunia hii, usisumbuke sana nenda kwenye maduka ya vitabu utanikuta humo. Ndio sebuleni kwangu. Pengine ninapopapenda nikiwa upande huo wa New York ni Schomburg Center for the Study of Black Culture. Nenda hapa.
Hiyo ni New York. Palipotokea yale maafa ya ile tarehe inayofanana na namba ya kuita mapolisi: 911 (yaani tare tisa mwezi wa kumi na moja.) Hivi wale jamaa waliopeleka yale madege kwenye lile jengo walichagua siku hiyo kutokana na tarehe hiyo kufanana na namba ya mapolisi au?
New York ndipo kijana Amadou Diallo toka Afrika Magharibi aliuawa na polisi kwa risasi 41 akiwa hana kosa lolote. Risasi 41! Mwanamuziki nimpendaye Bruce Springsteen alitunga wimbo uitwao American Skin (41 shots). Ukienda hapa unaweza kumtazama video ya Bruce akiimba wimbo huu na pia kusoma mashairi ya risasi 41. Ukifika katika tovuti hiyo, shuka chini hadi uone palipoandikwa AMERICAN SKIN VIDEO. Bonyeza hapo. Usisahau kufuatilia mashairi ya wimbo huo katika tovuti hiyo.
Nimekumbuka pia kuwa Jean Wycleaf aliyekuwa katika kundi la Fugees na Lauryn Hill alimuimba pia Diallo katika albamu yake ya Ecleftic. Soma mashairi ya wimbo huo uitwao Diallo hapa, ambao alimjumuisha Yossou N'dour na MB^2.
Pale Toledo, Ohio, nilipoishi miaka miwili sijui jinsi ya kupaelezea kwa kina. Iko siku. Leo nitagusia mambo mawili matatu: Mji wa Toledo ni mji dada wa mji wa Tanga. Kuna mahusiano makubwa ya shughuli za maendeleo kati ya miji hii miwili. Kwa mfano, kulikuwa na gari la zimamoto toka Toledo kwa mji wa Tanga kama zawadi. Sijui kama limefika. Pia shirika la Great Lakes Consortium , lililoko Toledo, lina miradi mbalimbali kupitia serikali ya Marekani na mpango wake wa AGOA wa "kusaidia" wafanyabiashara wadogo ili kuweza kupata masoko hapa Marekani. Mwaka jana wafanyabiashara kadhaa toka Tanzania walitembelea Toledo.
Pale Toledo kilichokuwa kinanitisha ni wizi wa kutumia silaha. Kila taarifa ya habari jioni unasikia fulani na fulani wamekamatwa wakiiba kutumia silaha. Fulani na fulani wameuawa na majangili. Duka hili na na kituo kile cha petroli (hapa petroli wanaita gesi!) vimeingiliwa na majambazi. Nilitishika zaidi wakati sheria ilipopitishwa ya kuruhusu wakazi wa mji ule kutembea na silaha zao mitaani. Hii nchi ambayo inajivuna kuwa mfumo wake wa sheria na utawala umejengwa juu ya amri kumi, ambazo Musa alidai kupewa na mungu, sijui kwanini inakuwa na upenzi mkubwa namna hii wa kubeba silaha badala ya biblia! Katiba ya Marekani inatamka wazi kuwa ni haki ya kikatiba kwa raia kubeba silaha. Ni haki ya kikatiba pia kwa raia kuunda majeshi yao binafsi. Na hayo majeshi yapo. Hili tutazungumzia siku moja.
Pale Toledo kuna mitaa ambayo barabara zake zinanikumbusha barabara za Tabata miaka ya nyuma (kabla hazijatengenezwa kama sasa.) Halafu watu pale washamba sana, hawajui dunia inakwenda wapi au imetoka wapi. Kila wanachoona kwenye luninga wanaamini. Ukiwatajia Afrika wanachoona ni vita, njaa, ukimwi, n.k. Nimekutana pale na watu wana mapengo, kwa kutokuwa na bima ya afya, wananiuliza juu ya tabu za Afrika, nawaambia, "Nilipotoka hakuna mtu ninayemjua mwenye umri kama wako ambaye ni kibogoyo!" Wakiongelea juu ya Afrika kuwa nyuma kiteknolojia, huwa ninawauliza mara ya kwanza kuwa na anuani ya barua pepe. Wengi hudhani kuwa ninadanganya ninapowaambia kuwa nilikuwa na anuani toka mwaka 1996-97, wakati wengi wao walikuwa wakisikia "email" kwenye bomba! Na situmii mfano huu kwakuwa nadhani kuwa hicho ni kipimo bora cha maendeleo ya teknolojia au kudhani kuwa maendeleo ya teknolojia ni sawa na maendeleo ya watu, hapana. Nataka kuwaumiza vichwa kwa kuwaonyesha kuwa mtazamo wao juu ya Afrika ni finyu sana. Wanaongelea juu ya sisi kuwa nyuma kiteknolojia wakati bila nambari 1 hadi 9 wasingekuwa na teknolojia waliyonayo leo. Na nambari hizi ni mababu zangu ndio waliowapa! Maaluni kabisa!

Hiyo ni tisa, kumi...nina hamu sana ya ugali kwa kisamvu cha nazi kwa mama ntilie, ndizi za mama pale Moshi, mtori kwa sana, chipsi mayai "zikaushe na weka kila kitu pamoja na ukwaju"(pale American Chipsi kinondoni au mitaa ya Kariakoo mida ya saa tatu usiku), juisi ya miwa pale Kariakoo au Buguruni kwa Wapemba, mbege ya Moshi, wali wa nazi kwa maharage kwa mama lishe....acha jamani. Nchi yetu...acheni tu. Tatizo letu ni hawa "viongozi" wetu wanaouza kila kitu kama vile wameishiwa akili.
Mwisho wa gumzo. Umechoka? Niendelee nisiendelee? Wanaotaka niendelee wanyooshe vidole...

0 Maoni Yako:

Post a Comment

Links to this post:

Create a Link

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com