2/20/2005

KISA KIFUPI: DUNIA IMEJAA WENDAWAZIMU

Maneno yaliyomtoka ni kama ya yule mwanamke asiye na makazi niliyekutana naye hivi majuzi. Alipomaliza kuongea nilijiuliza imekuwaje wakaniambia jambo hilo hilo? Wanafahamiana?
Yule mama ni mzungumzaji. Niliongea naye kwa dakika chache na toka siku ile sijamuona tena. Huyu bwana anapenda tu kutabasamu kwa chati. Akikusalimu, anakusalimu kwa haraka wala hakutazami machoni. Ukimsalimu, anakujibu kwa mkato. Inadaiwa watu wa kabila lake wako hivyo. Katoka kabila la wahindi wa asili ya Marekani la Navaho. Toka nimetambulishwa kwake wiki kadhaa zilizopita hajasema neno.
Lakini jana kafungua mdomo. Maneno yale yale ya yule mama: Dunia imepata wendawazimu. Kila mtu kawa kichaa. Tumepandwa na wazimu. Tumerukwa na akili. Nati zimechomoka. Walimwengu tunaokota makopo bila kujijua.
Kweli? Kwanini anasema hivyo? Nilimuuliza.
Sikiliza taarifa za habari. Alinijibu, akaendelea: Hivi ukitazama luninga unaona chochote siku hizi? Damu si imechafua kioo? Hivi risasi hazijawapata watangazaji?
Aliuliza huku akinitazama kama vile anasubiri jibu. Nilitumia nguvu zangu zote kujizuia kucheka. Sio kumcheka. Kujicheka mimi na walimwengu wenzangu lakini sababu hasa sijui.
Akaniambia: Usipende kuganda mbele ya luninga. Utakuwa mjinga. Kwanza ukitazama sana kuna siku bomu litakosa njia likuangukie sebuleni.
Nilijiuliza kama anayosema ni mafumbo au kuna tatizo akilini mwake.
Kisha akauliza swali jingine. Yale mengine sijamjibu: Hivi hawa jamaa bado wako Iraki au wameenda kwingine?
Alikaa kimya kidogo akinitazama kama vile hanioni, akaendelea: Bila bangi mimi nami ningekuwa kichaa tayari kama ninyi. Sijui mnaishije kwenye dunia yenu hii bila bangi!
Alitikisa kichwa huku akiondoka.
Hiyo ilikuwa ni jana. Leo hajasema lolote. Nikimtazama, anatazama pembeni. Nikimsalimu, anajibu kwa mkato. Nasikia ameacha kusoma magazeti, kusikiliza redio, au kutazama luninga.

0 Maoni Yako:

Post a Comment

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com