2/25/2005

TUBINAFSISHE IKULU!

Kwanza kabisa kwa wale ambao kiswahili kipya kinawapiga chenga: UBINAFSISHAJI = PRIVATIZATION
***************************************++++*****************************************
Nimeamua kabisa kuandika makala nzima juu ya mapendekezo yangu matatu ya nani awe rais wa Tanzania baada ya walaji walioko sasa hivi kumaliza kipindi chao mwishoni mwa mwaka huu. Moja ya mapendekezo yangu ni kubinafsisha ikulu. Kubinafsisha urais. Hili kuna watu wametaka ufafanuzi. Kwakuwa makala yenyewe haijatoka bado nchini Tanzania (hadi jumapili hii), sitaweza kuiweka hapa ukumbini. Ila hoja yangu kuu katika hili ni hii: tukishindwa kuendesha kiwanda tunafanya nini? TUNABINAFSISHA. Tukishindwa kuendesha mabenki tunafanya nini? TUNATABINAFSISHA. Tukishindwa kuendesha migodi (hata ile ambayo madini yake hayana ushindani wowote maana yanapatikana tu Tanzania kama vile Tanzanite!), tunafanya nini? TUNABINAFSISHA. Tukishindwa kuendesha viwanda tunafanya nini? TUNABINAFSISHA. Tukishindwa kuendesha TANESCO tunafanya nini? Tunaagiza uongozi mpya toka nje ya nchi.
Je tukishindwa kuendesha nchi tufanye nini? Tubinafsishe uongozi. Tubinafsishe ikulu. Tuwape wanaoweza kuendesha viwanda vyetu, mabenki yetu, mashamba yetu, migodi yetu (hasa wale wanaopeleka makontena ya mchanga Japani), n.k. Tuwape. Kama tumeshindwa kuendesha kiwanda cha nguo au benki au biashara ya madini ya Tanzanite yasiyopatikana nchi yoyote ile (kwahiyo hatuwezi kulalamikia ushindani), TUTAWEZAJE KUENDESHA NCHI?
Suala hapa ni nani wa kumpa. Mzungu yupi poa zaidi. Kaburu (mbaye anaitwa mwekezaji siku hizi)? Muingereza? Mjeremani? Mmarekani? Tumpe nani? Hili ndio bado linaniumiza kichwa.

0 Maoni Yako:

Post a Comment

<< Home

FREE hit counter and Internet traffic statistics from freestats.com